KATIBA NA KUJIMILIKISHWA VYAMA CHANZO CHA MIGOGORO

Posted: November 29, 2016 in Uncategorized

Tanzania ina vyama vingi vya siasa, ikiwa ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi, ambacho kilitokana na muungano kati ya vyama viwili vya Tanganyika African National Union (TANU) cha Tanganyika na Afro Shiraz Party (ASP) cha Zanzibar.

Vingine ni Civil United Front (CUF), Tanzania Labour Party (TLP), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na National Convention for Constitution and Reconstructon-Mageuzi (NCCR-Mageuzi).

Pia vipo vyama vya National League of Democracy (NLD), Democratic Party (DP), Alliance for Change and Transparecy (ACT-Wazalendo), utitili wa vyama vingine vingi.

Kwa muda mrefu Watanzania tumeshuhudia migogoro ndani ya vyama hivi vya upinzani tukianzia na NCCR-Mageuzi, CHADEMA na sasa CUF. Hivi ndivyo miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa sasa, umoja huo uliasisi wakati wa Bunge la Katiba, waliamua kuendelea kutumia jina hilo hata baada ya mchakato wa katiba kukwama. Inavunja moyo Watanzania wenye hamu ya mabadiliko ambayo wengi wamedhani yatakuja kupitia chama kingine chochote na si CCM wana migogoro isiyoisha. Migogoro mingi ndani ya vyama imekuwa juu ya madaraka ndani ya vyama hivyo, haianzii kwa wananchi, inaanzia kwa viongozi na hatimaye kwenye vikao vyao ambavyo wananchi hawahusiki. Mara vyombo vya habari huchukua hizi agenda za ugomvi wa viongozi na kuzileta kwa wananchi. Ambao nao huishia kuwa na mitazamo yao, hata hivyo huchagua upande katika pande mbili zinazoshindana na huo ama huwa mwisho wa umaarufu wa chama husika ama huzorota.

Leo hii tunashuhudia vyama hivi vya siasa vikipoteza mwelekeo kabisa, vyama havijui tena vinachokisimamia, liliko mbele yao ni ama kuendelea kubaki madarakani au kuingia madarakani. Wanaokuwa madarakani imekuwa ni vigumu kutofautisha shughuli za serikali na shughuli za siasa. Kiongozi wa serikali anafanya ziara ya kichama kwa kutumia nyenzo za serikali, viongozi wa serikali wanatoa maagizo ya kiserikali ndani ya vyama na kutoa maagizo ya vyama ndani ya serikali. Mstari uko wapi unaobainisha kuwa hapa na haya ni mambo ya serikali kama kiongozi wa serikali hurusiwi kufanya mambo ya chama chako ambayo ni kadha wa kadha. Mstari uko wapi unabainisha hapa na haya ni mambo ya chama kama kiongozi wa chama mambo kadha na kadha ya serikali hayaji huku.

Wanaotafuta kuingia madarakani nao imekuwa vurugu zaidi kwani wanaamini demokrasia inawaruhusu kufanya chochote ili kuingia madarakani. Mstari uko wapi unamwambia mwanansiasa kuwa ni amri kwa mwanasiasa yeyote kushirikiana na serikali iliyoko madarakani kuwaletea wananchi maendeleo. Inasikitisha kuona wakati wanasiasa waliochaguliwa na wananchi wanatakiwa kushirikiana na serikali iliyoko madarakani kuwaletea maendeleo kwa kuwasimamia na kuwashauri lakini ugomvi wa kuwania madaraka umeachwa bila kanuni wala sheria, wanasiasa wanageuka kupandikiza chuki miongozi mwa wananchi waichukie serikali yao. Serikali inapandikiza chuki kwa wananchi wachukie wanasiasa. Ni upumbavu wa hali ya juu kwetu sisi kuona mambo haya na sote tunaweka maslahi yetu binafsi mbele na kutafuta ni upi unaweza kunipatia mlo ndio unasapoti bila kurudi chini ukajiuliza ni vitu gani hivi tunavisapoti katika jamii yetu.

Tahadhali ichukuliwe ili kuepuka kujiingiza katika siasa za ugomvi wa ndani ya vyama au wa wanasiasa na serikali. Nikitafakari najiuliza, ni namna gani tunaweza kuleta mabadiliko katika nchi hii? Je ni kweli walio wengi wanataka mabadiliko au ni wachache tu ambao mara nyingi wanaitwa wasomi? Je mabadiliko haya ni ya muhimu, na kama ni ya muhimu kwa nchi yetu ni namna gani tutawasaidia wengine waelewe umuhimu huu wa mabaliko? Je, tusubiri chama fulani kiiondoe CCM ndio tuanze mabadiliko? Au wananchi tusukume mabadiliko tuyatakayo kila mmoja katika eneo lake?

Wengi tunaamini katika demokrasia, tatizo hasa ni demokrasia ya namna gani. Kuna walioona Libya haina demokarasia hilo halina ubishi. Ubishi wetu na nchi za magharibi ambazo ndizo zinadhani ni miamba ya demokrasia, ni jinsi ya kuleta demokrasia Libya, Iraq, Syria na kadhalika. Kuchukua nafasi ya CCM kunaweza bado kusitibu matatizo ya demokrasia ya Tanzania, ingawaje itakuwa dalili nzuri kwamba wananchi wanaweza kuamua jambo likatendeka. Hiyo ni dalili njema.

Tanzania tuna demokrasia ya vyama vingi hilo halina ubishi pia. Baadhi tunaona kwa sababu ya CCM kuendelea kutawala hatuna demokrasia kamili. Wengi pia hatuelewi kwamba Tanzania hatuna demokrasia ya vyama vingi tuna demokrasia ya CCM iliyoruhusu kuwepo kwa vyama na inayotoa imla ya namna gani ipingwe. Wanasiasa walioko upinzani ama wanalielewa hili au kwa kukinzwa na maslahi binafsi hawalioni. Katika vita yoyote ni muhimu kumfahamu adui yako: Ni nani, anauwezo gani, yuko wapi. Inawezekana kabisa adui wa vyama vya upinzani si CCM kama wengi wanavyodhani na ndiyo maana vinaenda hatua tano mbele halafu vinarudi hatua kumi nyuma. Chama tawala wanaliona hilo na ndio maana wanasema CCM itaendelea kutawala milele. Si kweli lakini bila upinzania kujua nani hasa wanampinga itachukua muda kukamata dola.

Ugomvi ndani ya vyama wa hapa na pale ni wahusika kupoteza picha kubwa na kukosa kuunganisha na mawazo ya umma na tamanio lake. Wanajiona wenyewe hawaioni nchi na shida yake. Nashauri wapinzani wote wadogo na wakubwa wajiulize wanampinga nani hasa?

Kwa mfano swala la CUF, si kweli kwamba kumwondoa Profesa Lipumba katika uongozi wa chama na kumweka mwingine yeyote kutaimarisha demokrasia ndani ya CUF na hatimaye kuwa mfano bora na kujenga imani kwa wanachama na wananchi ambao ndio wapiga kura. Kwamba kumtoa Lipumba kutatoa picha kwa wananchi kwamba CUF inaheshimu demokrasia na hivyo inafaa na kuaminika. Si rahisi kiasi hicho!

Ni kweli kiongozi yeyote anatakiwa kuheshimu taratibu walizojiwekea lakini si sahihi kudhani kwamba tatizo la Chama Cha Wananchi CUF ni Profesa Lipumba, Maalim Seif na wengine tu. Tatizo si yeyote miongoni mwao, tatizo kubwa ninaloliona ni watendaji kutosoma KATIBA yao, lakini tatizo hilo huenda miongoni mwao hawalijui na ndiyo maana Mzee Lipumba katumia udhaifu huo kutaka kurudi madarakani.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) huwa wapo makini sana kwenye kukabiliana na migogoro ndani ya chama tofauti na vyama vingine. Turejee mgogoro wa kina Samuel Sitta (Mungu amlaze mahala pema) na Edward Lowassa jinsi ulivyomalizwa bila ya kufukuzana, ni ishara kuwa kuna taratibu ambazo wao wamejiwekea. Migogoro ndani ya vyama ambayo imekua ikihusisha viongozi kwa kukumbuka michache kuna Dokta Walid Kaborou dhidi ya Chadema, Chacha Wange (Mungu amlaze mahala pema) dhidi ya Chadema, Zitto Kabwe dhidi ya Chadema, Hamad Rashid dhidi ya CUF na David Kafulila dhidi ya NCCR-Mageuzi ni migogoro ambayo imekwamisha vyama au imevizorotesha.

Pia umiliki ndani ya vyama unaonekana kushamili na kuibua migogoro kati ya wamiliki na wanaotaka nafasi za juu za uongozi. Kwa uchache migogoro kama ya Marehemu Chacha Wangwe na Zitto kwa Chadema ilihusisha umiliki. Ninapoongelea umiliki namaanisha kuna watu ambao wanaona wao nafasi zao ndani ya vyama haziguswi, haziwezi kugombewa na watu wengine hadi wao watoke madarakani kwa muda wanaoutaka wao waliojimilikisha na ukiwagusa huwa inaleta kelele sana na hiyo ndio iliyowaondoa Zitto Kabwe na Wangwe. Pia mgogoro wa sasa wa CUF vita kuu ni umiliki, maalim Seif anajiona ni mmiliki wa CUF hawezi kuguswa anajiona ana madaraka yote ya kuamua anataka kufanyakazi na nani na nani hamtaki. Umiliki umeleta athari kubwa kwa vyama maana wenye nafasi hizo hawatoi nafasi ya mawazo mapya ndani ya uongozi. Umiliki umekua ni chanzo cha kupoteza lengo kuu la kupambana na chama tawala katika kuelekea kukamata dola, nguvu nyingi zimewekezwa

Je hatuwezi kufanya siasa za ustarabu ndani na nje ya vyama kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake bila kumchafua au kumharibia mwenzake?

Nakutakia usomaji mwema.

Twitter @noor_abdul

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s