CCM ILIJIANDAA KUSHINDWA KULIKO KUSHINDI

Posted: November 25, 2016 in Uncategorized

Katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, CCM ilikuwa imejiandaa zaidi kwa ajili ya kushindwa kuliko ushindi. Kama chama hawakutarajia kushinda na ni wazi hawakuwa na agenda ya ushindi zaidi ya kuokoteza hoja kutoka kwa wapinzani. Hii imenikumbusha filamu iliyochezwa Mwaka 1972 inayoyojulikana kama The Candidate kibongobongo tuite ‘Mgombea’. Bwana Robert Redford aliigiza kama Bill Mckay kihiyo wa kisiasa ambaye alijikuta anaingia kwenye kinyang’anyiro cha Seneti ya Marekani na kushinda akiwa hajui nini kinafuata baada ya uchaguzi.

Akiwa hana nafasi yoyote na hatarajii kushinda bali kushiriki akajikuta anapita katika hatua mbalimbali za kinyanganyiro. Bila kutarajia Mckay anapewa mkono huru kusema lolote atakalo juu ya kisiki kilichokua mbele yake. Kwakua hakujiandaa na ushindi alianza kupumua kwa kutweta. Hata hivyo, kama matokeo ya mfululizo wa maendeleo asiyotarajia, kura zake ziliendelea kupanda katika uchaguzi huo na kumpa matuaini. Siku ya uchaguzi kwa mshangao wa kila mwananchi, yeye (Mckay) alimuacha mbali mpinzani wake wa karibu, alipata ushindi wa kimbunga na kuchaguliwa kuwa Seneta wa Marekani.

Utamu wa filamu ni usiku wa siku ya uchaguzi wake. Baada ya kusikia ameshinda, Mckay alichanganyikiwa na kujiona kama hakustahili. Kwa hakika ushindi haukuwa sehemu ya mpango wake. Kama kawaida vyombo vya habari na watu wengi waliofuatilia kwa karibu walikuwa na hamu ya kutaka kujua amepokeaje majibu ya ushindi wake wa kishindo, akiwa mbele yao alichofanya alimuita meneja wa kampeni zake ndani ya chumba na akamuuliza kutoka moyoni mwake: “Marvin, tunafanya nini sasa?” Kabla Marvin hajajibu, vyombo vya habari vya karibu vilivyokua vinaonyesha vikawatoa nje ya chumba na filamu ikafika mwisho.

Utamu wa filamu hii uliifanya kupokea tuzo za Oscar kama Best Screenplay ya 1972, inawezekana kuwa Mckay alifanikiwa kwa kuwafanya wapiga kura wajinga na kumpigia kura kwa wingi, hakuwa na fununu nini cha kufanya kama Seneta wa Marekani. Alichukulia kama utani na kutimiza alichotaka lakini utani ukamgeukia yeye. Hakutarajia kushinda na hakuwa na mpango wa dharura wa ushindi wake.

Ukimfikiria mgombea Bwana Mckay inawezekana ni mzaliwa au alipata wazo hilo kwa urahisi kutoka Tanzania maana uchaguzi wa 2015 hauna tofauti na “Mgombea” ya mwaka 1972.

Katika muktadha wa Mckay, CCM ukiitafakari kwa undani unaona ushindi kwao haikua dhamira kuu bali janga dhidi yao. Hii inadhihirisha hali inayoendelea kwa sasa Tanzania. Ukitaka kuitafakari Serikali ya CCM na majibu ya matatizo yetu kwa sasa, ni kwamba utagundua serikali inaona kuna mdororo wa kiuchumi lakini haina majibu ya nini kifanyike.

CCM haikuwa na mpango baada ya ushindi.

Baadhi ya wanachama walizunguka sana kwa Watanzania kuwaomba ridhaa ya kuwaongoza na waliona wanayo mawazo mapya yaliyotarajiwa kuongozwa na Daktari Magufuli lakini wengi wao pia walishapoteza dira na walishakuwa watu wakujiona wao ni wao sambamba walitegemea serikali ingeweza kuanzisha labda tuite muelekeo mpya wa kujiondoa kwenye tope la muda mrefu la kuona na kuwaza kama tuko karne ya kumi na sita. Lakini katika serikali hadi sasa hakuna ufumbuzi juu ya jinsi gani wanaweza kushughulikia matatizo ya dharura ya uchumi wa Tanzania.

Pengine mtu anaweza kueleza ukweli kwamba, katika mazingira ya mtikisiko wa kudorora kiuchumi, CCM wamekua wapiga zumari wazuri wa kutetea hoja za kiongozi wao hata kama wanaona tunakoelekea ni shimoni. Kuna marafiki zangu wana CCM ambao huwa tunabishana nao ila napenda misimamo yao baadhi hawaongozwi na kunywa maji ya bendera. Mfano Serikali ilipokuja na “Nahamia Dodoma” wakijua haikuwa katika ilani yao wala katika sera zao na wakijua bajeti ya mwaka 2016/17 imepitishwa bila kugusia, je mwana CCM anaekuja na hoja hii mufilisi anakushawishi vipi kuwa wanaweza kutekeleza yale waliyoahidi kama hawajui kipaumbele ni nini? Naamini nia ya kuhamia Dodoma ni njema na toka utoto tumekua tunaisikia na kuiunga mkono lakini kila kitu kitimizwe kwa wakati wake. Tukitaka kujua kuwa ajenda ya kuhamia Dodoma ni kaa la moto naomba uniambie Waziri Mkuu alipotangaza kuhamia Dodoma na akafanikiwa mwishoni mwa Septemba kama alivyoahidi je pale ofisini kwake Magogoni ni akina nani wamefuatana nae? (Kwa wana CCM mkinitajia kwa majina au vyeo vyao nitafurahi japo naamini hakuna hata mmoja). Hajaambatana na watendaji wa ofisi yake kwa sababu ya fedha kutokuwepo. Tujihoji kila siku tunatangaziwa makusanyo yanaongezeka, zile hewa zimeondolewa kila mahala, kwa nini PM ahamie Dodoma peke yake bila watendaji? Ofisi ya Waziri Mkuu imefanywa kama duka la Mangi akiamua kufunga yeye akiamua kufungua yeye kwa sababu ni jeshi la mtu mmoja. Ujinga wetu wapiga kura wa Tanzania tunashindwa kuuliza wapi CCM wana matumaini ya kupata fedha kwa ajili ya kutimiza ahadi zao kwetu, matokeo yake tunawapa kura mwisho wa siku kila kitu kinakuwa kimesimama.

Kwa sababu CCM hawakuwa na uhakika wa kuongoza serikali, hakuna maandalizi yaliyofikiwa na chama namna ya kurithi jinsi ya kutekeleza mipango iliyanzishwa na mtangulizi wake.

Kwa sababu CCM hawakuwa wanatarajia kutawala tena na hawakuwa wamejiandaa kutawala tena, ilimchukua Rais Magufuli miezi miwili ya kuchagua baraza lake la mawaziri.

Miezi miwili ya mipango ilitakiwa kuwa imezaa matunda yanayoonekana kwa wananchi hadi sasa. Wakati Watanzania wakitafakari kuchelewa kutangaza Baraza la Mawaziri wengine tulidhani alifanya hivyo akihitaji kupata watu makini, watakatifu na malaika katika Taifa hili. Lakini watakatifu na malaika wakageuka kuwa wale wale washindani wake kwenye kinyanganyiro cha urais katika chama chake.

Wakati rais akijisifu kusimamia serikali inayokusanya makusanyo makubwa zaidi, uchumi polepole unatoka kuwa wa kawada kuelekea mbaya na wawekezaji wanapiga mahesabu namna bora ya kutuacha katika hali ambayo Tanzania imekua ya Kodi, kila kitu kimekua kinakatwa kodi hata vitu ambavyo havistahili. Amenikubusha #SimCardTax tulipoipigania hadi kutopitishwa, sasa naiona inakuja kwa njia nyingine.

Wasaidizi wa Rais

Sasa ni dhahiri Watanzania tunakabiliwa na ukweli kwamba tuna wasaidizi hewa kwenye wasaidizi wa karibu wa Rais. Wanahitajika wasaidizi wa Rais kufanya kazi kwa kujitoa, inasikitisha hata sehemu ambayo Mawaziri wanaweza kumulika na kupashughulikia Rais ndio anaenda na kutumbua, siamini kama baadhi ya mawaziri wanafaa kuendelea kua kwenye nafasi zao, tumepoteza rasilimali nyingi kwa watangulizi wao,  ambazo zingetufanya tusiwe hapa tulipo leo, ukilinganisha thamani ya rasilimali iliyopotea na umri wa Taifa hili utaona kuwa badala ya kwenda mbele tulizoea kurudi nyuma, Mawaziri wa sasa wasiturudishe huko, tusisubiri Rais kugundua mabaya yaliyopo kwenye Taasisi na Idara za Serikali, muda wa kulindana tuuone kama uliondoka na awamu iliyopita, tusimpe Rais kazi ya kuteua na kutengua baada ya kuona mtu hafai kwa muda mfupi, wajaribu kushughulikia kwa haraka masuala kwa karibu kwa ajili ya kuweka utofauti wao na watangulizi wao.

Pia wanamuangusha Rais ni wote wanaopenda kumsifia badala ya kumwambia ukweli, kuna wasaidizi wanafiki wasiofikisha ukweli bali kumwambia yale ambayo hupenda kuyasikia na kufurahisha nafsi yake badala ya kuwa wakweli.  Kuwa kiongozi mwenye dhamana ya watu ni zaidi ya kuwa kada mtiifu wa CCM. Kuna haja ya kupima vigezo vya uteuzi kwa wasaidizi au wateule wa Rais siamini kama UKADA unatosha tu kumfanya mtu kiongozi. Imefikia hatua ambayo viongozi hawaaminiani kati yao unakuta Mkurugenzi wa Wilaya na Mkuu wa Wilaya hawaelewani, Mkuu wa Mkoa na Kamanda wa Polisi Mkoa wanavita ya madaraka, “sabotage” haiwezi kukosa kama tunao watu wa aina hii. Huko mikoani hali si shwari, wapo wakuu wa wilaya wamejifanya kuwa wanajeshi kwa kofia ya Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama na kutamba na silaha mchana kweupe. Utawala wa Magufuli wa kuteua makada umeleta ombwe kubwa la kiuongozi  kati wa vongozi wa kisiasa na wateule wa Rais. Imefikia mahala wapo makada wa CCM wanaochukizwa na kuomba nafasi za kisiasa zisingekuepo hasa zile zinazoongozwa na wapinzani na teuzi zake zilikua maalum kwa ajili ya kudhibiti wapinzani. Ila niachokiona mtaani ni kuwa kuendelea kukimbizana na wapinzani, kuwafunga kwa kesi zisizo na kichwa wala miguu wakidhani wanawadhoofisha ni kujidanganya maana wanazidi kuwaimarisha.

Tanzania ni mgonjwa, mgonjwa ambaye kwa sasa amelazwa katika wodi ya hospitali kwa ajili ya matibabu ya dharura. Hali yake ni mbaya. Upasuaji wa haraka unahitajika kwake. Hata hivyo, inaonekana daktari wa zamu hayupo. Muuguzi wa zamu wa usiku katika hospitali hufanyakazi kwa muda (part time). Mchana anavipaumbele vyake kwa ajili ya kuhudumia anaowataka. Wauguzi wengine pia ni sehemu ya wafanyakazi wa muda. Wao ni mkusanyiko wa wapishi, mafundi washonaji na wauzaji wa karanga, mama lishe, machinga na boda boda.

Hii inaibua wasiwasi mkubwa juu ya hatima ya mgonjwa. Ni nini kinaenda kutokea kwa Tanzania? Kama hatutakuwa makini, mgonjwa huyu anaweza kupata madhara. Wakati Rais Magufuli anateua Mawaziri wake aliamua kuchagua alioona wanamfaa hasa wapiga zumari “noise maker” ambao hadi sasa pamoja na mapambano wengi hawaonyeshi udhati wa kasi inayoridhisha.

Kumekuwa na vita ya maneno na miongozo mingi wakati wote, imekuwa kawaida kupuuza wachumi na wachumi hao hao wamejiingiza kwenye propaganda za kisiasa zisizo na uhalisia. Moja ya mambo ya ajabu kuhusu serikali hii ni kwamba inakataa kukaribisha hoja za wengine hasa wapinzani ili ziweze kutengeneza mazingira ya kujifunza. CCM wanakataa kukubali kwamba baada ya miongo kadhaa madarakani hawawezi kujinasua kwenye hali mbaya za wananchi wao, wamewafanya rasilimali ya kutimiza matakwa yao.

Rais Magufuli hakuwa na mpango maalum baada ya ushindi wa kuiongoza Serikali baada ya uchaguzi mwaka 2015 …. Watanzania wanaweza kuona na kutathmini kuwa pamoja na mambo mengine wanatambua na hasa baada ya kutokua na kauli ya kupinga ufinyangaji wa demokrasia kule Zanzibar, pia hakuna njia inayoonyesha ufumbuzi wa jinsi gani anaweza kushughulikia matatizo ya uchumi wa Tanzania nah ii inaonyesha dhahiri kuwa CCM ilikuwa imejiandaa zaidi kwa ajili ya kushindwa kuliko ushindi. Kama chama hawakutarajia kushinda na ni wazi hawakuwa na agenda ya ushindi zaidi ya kuokoteza hoja kutoka kwa wapinzani.

Twitter @noor_abdul

Advertisements
Comments
  1. thobias wolstani says:

    niukweli nando mahana akuna cha kujivunia ktk maisha toka umeisha uchaguzi,ndo mazara asi ya kuiga sera za mtu pasipo kujua wapi utapata ili utimize ulicho haidi kwa watu walo kuchagua .

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s