Magufuli Anajenga kwa Kubomoa

Posted: October 5, 2016 in Uncategorized

Rais Magufuli kwa maamuzi na hatua ambazo amechukua ni dhahiri kwamba anataka kujipambanua na awamu za uongozi zilizopita. Ajenda yake kuu ya kupambana na ufisadi imemfanya aharakishe michakato wa kuanizishwa kwa Mahakama ya Mafisadi licha ya matatizo mengi yakiwemo kuchambua matatizo yatokanayo na mifumo ya utendaji kazi ndani ya serikali badala ya kufikiria kwamba yote yanayotokea ni udhaifu wa binadamu. Dalili zinajionyesha kwamba Rais Magufuli anataka kuanzisha utawala wa amri moja. Hilo limejidhihirisha kwa watu anaowateua ambao wengi wao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi, Wanajeshi na Polisi. Vile vile ameteua MaProfesa na MaDaktari wa falsafa katika nafasi mbalimbali za utumishi wa uma akiamini juu ya uelewa wao kuwa mkubwa kuliko wale waliokuwepo.

Rais Magufuli anauona upinzani kama kundi la wachochezi badala ya kuutambua kama nguzo muhimu katika ujenzi wa demokrasia na uongozi mbadala ambao unakuwa na haki zote za kuendesha uongozi na utawala wa nchi.

Amezuia safari za nje kwa madai kwamba ni kupoteza fedha na wakati huo huo akiamrisha kwamba maombi yote yanayohusu safari za nje yapelekwe Ikulu na yeye au Ofisi yake iyapitie na kutoa kibali.

Katika kubana matumizi Rais amekataza kufanyika sherehe zozote zikiwemo za Muungano na Uhuru japo ni sherehe muhimu sana katika historia ya nchi hii.

Ametamka wazi kwamba watu wazae badala ya kutumia uzazi wa mpango. Alitumia dhana ya “kufyatua” watoto kama kufyatua matofali. Kwa kuwa elimu ni bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari. Lakini mpango wa uzazi ni zaidi ya kufyatua watoto. Kuna afya ya mama na mtoto, masuala ya kukua kwa uchumi na kuongezeka kwa idadi ya watu na pia uwezo wa watu kulea (kwa kuwapa watoto malezi bora). Rais Magufuli kwa suala la kufyatua watoto kwa kiasi kikubwa kapotea njia. Hii ni namna anavyotamka mambo mazito bila kufikiria athari zake.

Jambo lingine ambalo naona haliko vizuri ni suala zima la mishahara mikubwa kwa baadhi ya watendaji wakuu wa mashirika ya umma. Nakumbuka miaka ya hivi karibuni tumekuwa tunaona wataalamu kuhama kutoka sekta binafsi na kwenda serikalini, jambo ambalo kwa miaka mingi lilikuwa kinyume, kwani watu walikuwa wanatoka serikalini kwenda kwenye sekta binafsi ambapo maslahi yalikuwa yameboreshwa. Rais amesema wanaopata mishahara mikubwa itapunguzwa. Lakini watu hao hawakuja kufanya kazi za kawaida, bali wameleta taaluma, weledi, maarifa na ubunifu kiasi cha kuyafanya mashirika ya umma yaliyokuwa yameanza kufilisika kuanza kuwa na uhai na kufikia kuanza kutengeneza faida. Hivyo lazima kukubaliana na ukweli kwamba wale wanaopata mishahara mikubwa wanastahili japo inaweza isiwe katika ukubwa huo unaotajwa kwa sasa.

Kuhusu mpango wa Rais wa kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda naona kuna mapungufu mengi. Jambo hili ni kubwa, Rais anatakiwa kufanya mashauriano ya ndani na ya nje kuhusu namna ya kutekeleza mpango huu. Kubwa zaidi ni kwamba, mpango uonyeshe jinsi nchi inavyoweza kutumia rasilimali zake, kuinua viwanda vidogo viwe vya kati na vya kati viwe viwanda vikubwa. Lakini tujiulize swali gumu bila kusafiri kujifunza kwa wengine tutafikaje hapo tunapopataka?

Mapinduzi ya viwanda nayategemea matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji. Pia utoaji mafunzo ya ujasiliamali na ubunifu. Na vilevile kutengeneza bidhaa zenye ubora, bei nafuu kwa hapa nchini na nje. Mapinduzi ya viwanda siyo kutegemea viwanda vikubwa tu ambavyo vitakuwa vya kigeni.

Tujikumbushe historia ya namna ya kupata mgombea ndani ya CCM iliyopelekea Mtukufu Rais kupatikana tukianzia enzi za Baba wa Taifa. Zoezi la kuteua mgombea katika Chama Cha Mapinduzi kwa muda mrefu limekuwa na maana kubwa kwa kumaanisha kwamba yule anayeteuliwa anakuwa na uhakika mkubwa wa kuwa Rais.

Wakati tunajifunza siasa kwa waliotutangulia tulisikia historia nyingi za siasa za nchi yetu. Tulisikia mengi juu ya muasisi wa Taifa letu. Kutokana na historia hizo naamini toka Mwalimu Nyerere ang’atuke mwaka 1995, harakati za wanachama wa CCM kutaka kugombea Urais, vimeleta vuguvugu na ushindani ambao chama hakikuzoea huko nyuma. Mwalimu Nyerere hakuwa na mpinzani na nadiriki kusema hakuwa na mshindani pia. Niliwahi kusoma mahala jinsi vijana walivyokuwa wanalinda ofisi ya Katibu Mkuu ili kuhakikisha kwamba hakuna mwanachama au mtu anachukua au kurudisha fomu za kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama dhidi yake (Mwalimu Nyerere). Waliotaka kurithi nafasi ya Mwalimu Nyerere mwaka 1985, Mzee Mwinyi na Dkt. Salim walishindana na kupimwa kwa misingi ya kujitambulisha na Mapinduzi ya Zanzibar 1964 na kuungwa mkono na kundi lipi upande wa bara. Hiyo ndiyo ilikuwa ajenda. Mwalimu Nyerere aliyemtaka Salim alishindwa. Mwinyi kama Magufuli, ambaye awali hakuungwa mkono na Mwalimu Nyerere bila kuwa na nafasi ya juu ya uongozi wa kitaifa katika Chama Cha Mapinduzi alishinda.  Tangu wakati ule, siasa za Tanzania bara na visiwani zilichukua mkondo wa kipekee.

Upekee wa siasa ndani ya chama tawala ulikuwa ni kujitokeza kwa siasa za makundi yanayopingana, matumizi ya fedha na Mwenyekiti wa Chama ambaye ni Rais wa nchi na Mkuu wa Serikali kutaka kuwa na kauli kwa Rais ajaye. Wakati huo huo, mataifa ya kigeni yalikuwa yanafuatilia sana kuhusiana na Rais ajaye.

Kuhusiana na mpangilio wa nguvu za ndani ya nchi, udini, ukanda na kuwepo vyama vya upinzani, vyote hivi vilichangia kupandisha joto la ushindani ndani ya Chama.

Tofauti na mawazo ya wengi Mwalimu Nyerere alitumia hoja ya Lowassa na Kikwete kutaka kugombea Urais kama silaha dhidi ya Malecela. Mwalimu hakumtaka Malecela kwa sababu alimuona kama “kibaraka” wa Waingereza na Kanisa lao la Kianglikana. Nyerere alifanya kazi kubwa ya kumwondoa Malecela katika kinyanganyiro.

Baada ya chama hicho kuuzika ujamaa na kukumbatia ubepari matumizi ya fedha kuwanunua wajumbe yaliongezeka. Makundi ya wafanyabiashara (ndani na nje ya nchi) yalitaka kumweka mtu wao. Ni wazi serikali za Uingereza, Marekani na baadhi ya serikali za Umoja wa Ulaya zilimtaka Malecela kwa sababu ni mwanadiplomasia mahiri na haonyeshi kunogeshwa na siasa za kishoshalisti. Vile vile, alipokuwa Balozi Uingereza alijenga ukaribu wa serikali ya Uingereza na Wafanyabiashara wa Kiasia, wengine ambao walitoka Tanzania kuhamia kule na wana maslahi Tanzania. Kama Waziri Mkuu wa Serikali iliyoongozwa na Rais mwinyi, aliwapa biashara kubwa wafanyabiashara wa kuingiza magari na wengine ambao walihusiana na uwakala wa silaha kwa ajili ya majeshi ya ulinzi na usalama.

Mkapa alishinda kwa sababu Nyerere alimfitini Malecela na kumtumia Kikwete kama silaha ya kuwazuia Umoja wa Vijana wasimuunge mkono Malecela (ambaye tayari alikwisha wanunua).

Kujitokeza kwa wagombea wengi mwaka 1995 kuliashirikia mwanzo wa makundi maslahi na siasa za mitandao. Hayo makundi maslahi yanakuwa na taswira ya kipekee kwamba hata baada ya uchaguzi yanaendelea kuwepo na yanajitokeza kushindana na kupambana ndani ya chama tawala na jumuia zake na ndani ya serikali. Vita ya makundi iliendelea kuwa vita ya kudumu.

Mwaka 2005 Kikwete aliteuliwa na Chama tawala CCM kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya chama hicho. Kikwete alikuwa amefanya matayarisho ya kutosha, alikuwa anajuliakana kwa viongozi wakuu, wanachama na viongozi na pia kwa uma mzima. Alikuwa na wapiga kampeni wenye uwezo (Lowassa na Rostam) ambao walikuwa na fedha na pia walijua wapi pa kutafuta fedha za kampeni. Hata hivyo zilipikwa mbinu za kumwengua kama ilivyotokea kwa Lowassa. Wakati Kikwete aliruka vihunzi vya msaada wa Lowassa na wengine, mwaka 2015 Lowassa alitoswa na akaamua kujiunga na upinzani, akijiunga na Chama Cha Demokrasi na Maendeleo- CHADEMA (chama ambacho naamini katika misingi ya kuanzishwa kwake japo si mwanachama hadi sasa).

Kampeni za mwaka 2005 zilitawaliwa na kukolezwa na siasa za makundi za mitandao (mtandao mkubwa ukiwa wa Kikwete). Alishinda uchaguzi lakini athari za mchakato zimekivuruga Chama Cha Mapinduzi na Utawala Bora. Kitu ambacho kimejitokeza ni kwamba siasa za makundi, udini, ukanda, rushwa na kukosekana dira ya uongozi ndivyo vinatawala.

Mwaka 2015 siasa za makundi, vita dhidi ya Lowassa, matumizi ya makundi na kura za chuki zilimpa Magufuli uongozi.

Baada ya kugusia mambo yaliyojiri tangu mwaka 1985 wakati Mwalimu Nyerere alipostaafu mpaka 2015 tuangalie jinsi Rais Magufuli alivyo ukubali uongozi na changamoto zake.

Kwanza, mbinu za Magufuli katika kampeni zilikuwa kwamba CCM ni chama chenye mgogoro wa uongozi. Hivyo wapiga kura wamtazame yeye. Kwa kuikana CCM kulimwezesha kubeba ajenda ya upinzani ya kupambana na ufisadi. Lowassa alitumiwa kama rejea kwa suala la sakata la Richmond; kibao waligeuziwa wapinzani kwamba kwa kumkubali Lowassa walikuwa wamekubali kukumbatia ufisadi na mafisadi. Lakini hoja ya ufisadi ni zaidi ya mtu mmoja Lowassa. Na watu makini wamehoji kwa vipi ufisadi umeendelea kuwepo na kuongezeka maradufu tangu Lowassa aondoke serikalini? Matukio yaliyorejewa ni yale ya EPA, ESCROW, NSSF, NIDA, Makontena kupitishwa bandarini bila kulipiwa ushuru na mengine mengi katika Taasisi nyingi za uma.

Alipoingia serikalini, alianza na safari za kutembelea Taasisi na Wizara za Serikali kwa kushtukiza. Alikuwa anategemea habari za kuambiwa na wapelelezi au wana usalama ambao hawawezi kuunganisha au kutenganisha matatizo na mapungufu ya muundo na mfumo na matatizo ya utendaji kwani wengi wanachojua na kutaka kuonyesha umahiri wao ni kumkamata mwizi! Leo hii dhana ya kutumbua majipu inaonekana kuwa dhana pendwa kwa sababu inatoa maelezo rahisi kwa mambo magumu. Njia anayotumia ya kuamini anachoambiwa na kutaka kile anachojua na kutaka kitekelezwe vivyo hivyo, kuna uwezekano mkubwa aka”feli”

Tukio jingine ambalo hadi sasa sijapata “justification” ni uhusiano wa Bunge na Serikali. Rais Magufuli anaona bunge kama uwanja wa uasi. Fikiria; Magufuli anamteua Dkt. Tulia kuwa Mbunge na kumpendekeza awe Spika wa Bunge! Bunge linakatisha matangazo ya moja kwa moja ili kuzuia mambo na hoja za upinzani zisionekane. Baada ya hapo Rais anakataza mikutano ya hadhara. Magazeti yanafungiwa eti kwa kuandika mambo yasiyostahili. Hoja yangu ni kwamba mtu anayekuwa Spika au Naibu Spika, anapaswa kuwa amekaa Bungeni kwa muda mrefu (walau miaka kumi) ana uwezo wa dhahiri wa kuongoza, anajua siasa, usuluhishi na diplomasia, Je Daktari Tulia anayo hayo? Siamini kama kwenye utaratibu au kanuni za kumpata Spika au Naibu Spika hazitaji awe amekaa bungeni muda gani? Kama hazijataja nadhani hilo ni pungufu kubwa linaloweza kuzaa uwekaji mtu kwa maslahi fulani.

Yote haya yakiunganishwa yanaonyesha jinsi Mtukufu Rais anavyotaka kudhibiti upinzani ndani ya Bunge, ndani ya vyama vya Upinzani na pia ndani ya Chama tawala.

Kuhusu Sera ya nje; sera ambayo Magufuli amejitambulisha nayo ni kuwa karibu na Rwanda kuliko jambo jingine. Tanzania haijihusishi kwa kina na masuala ya Jumuia ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Afrika. Mpaka sasa Rais (ambaye kimsingi) ndiye ngama ya sera za nje ya nchi, amekaa kando. Hafanyi mashauriano ya mara kwa mara na viongozi wenzake nje ya nchi, kwani hataki kutembelea nchi za nje (sina uhakika kama ndio anabana matumizi au anaona atapoteza muda). Nijuavyo mimi, ni kwamba viongozi hukutana na kubadilishana  mawazo kuhusu masuala nyeti kama namna bora ya kukuza uchumi, namna ya kupambana na ugaidi au viashiria vya ugaidi na hata kukaribisha uwekezaji na masuala mengine kama mabadiliko ya tabia nchi, nakadhalika, yanakuwa ni matukio ya msingi. Tanzania siyo kisiwa na hakuna mtu ana haki ya kutumia hisia zake (bila mashauriano) kutekeleza sera na kuzingatia yanayotokea ndani tu bila kujali mambo ya nje. Kama watanzania wenyewe wana shauku kumwona Rais wao yukoje, vile vile wa nje nao wana shauku ya kumwona Rais Magufuli yukoje na wanawezaje kufanya kazi pamoja.

Masuala mengine ambayo ni matamshi ya kisera au maelekezo ya nini kifanyike; ni pamoja na kuleta Mapinduzi ya Viwanda na Serikali ambayo Wizara zake zote zina Makao Makuu Dar es Salaam kuhamia Dodoma.

Licha kwamba ni miaka 42 tangu serikali ilipodhamiria kuhamia Dodoma mpaka sasa ni Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI) pekee ndiyo ina Makao Makuu yake Dodoma. Matamshi ya Rais kwamba serikali ihamie Dodoma mara moja ni matamshi ambayo hayakufanyiwa uratibu. Wazo la serikali kuhamia Dodoma halikufikiriwa wakati wa kikao cha Bajeti 2016/17. Hivyo serikali itapaswa kutafuta fedha za kuwahamisha watumishi kwa kupunguza bajeti kutoka mafungu yaliyopitishwa kwenye bajeti. Pia kutakuwa na gharama za kijamii zitakazozikumba familia zitakazolazimika kuhamia Dodoma kwa amri ya serikali. Kuna familia zenye watoto wanaosoma shule za msingi na wanandoa wengine wote ni watumishi ama wa idara za serikali au sekta binafsi. Itakuwaje mmoja atakapohamia na mwingine ahami?

Nimalizie kwa kusema kuwa naunga mkono serikali kwa jitihada inazozinyesha ila kuna mapungufu niliyoyaanisha. Rais Magufuli katika kipindi kifupi ameleta vuguvugu la watu kumkubali kwa kukabiliana na matatizo ya ufisadi, uvunjifu wa sheria, ubadhirifu wa mali za uma na matumizi mabaya ya madaraka. Kuna watu wanamuunga mkono kwa hatua zake na kuna wengine hawakubali.

Kwa yale ambayo anayafanya kwa kuzingatia sheria na mgawanyo wa madaraka watu watakubali. Yale ambayo anatenda kwa hisia zake, ambapo yeye anakuwa askari wa kuwakamata wahalifu, yeye ni hakimu na yeye ni magereza watu watakataa. Na sasa ndivyo ilivyo.

Nawatakia usomaji mwema wa makala zangu, ningeomba kusisitiza maoni yako ni muhim kwa ajili ya kuboresha makala zijazo ila pia maoni yako nakuomba uyatoe chini ya chapisho hili ili kuwa na kumbukumbu sahihi tofauti na facebook au twitter.

Advertisements
Comments
  1. Thobias wolstani says:

    hongera kwa kuchanganua mambo kwa kina,kulingana na ukweli na mwerekeo wa nchi yetu ki uchumi,kisiasa na kijamii. nivyema mtukufu raisi akatumia sana mawazo na ushauri ya wapinzani na tahasisi nyingine ktk kuliletdaj maslai taifa na sio kuukandamiza na kuunyima uhuru kwa wote lengo ni kujenga nchi yetu.
    mungu ibariki tanzania.

    • Abdul says:

      Asante sana Thobias. Vijana walio wengi naamini wana mawazo mazuri ambayo yanaweza kusogeza nchi hii mahala fulani lakini wamekua na tamaa ya madaraka kwa kuwaza nafasi za uteuzi za Mtukufu Rais na kujiegemeza zaidi kwenye UKADA na kushindwa kutoa mawazo yao na kulifanya Taifa hili kusonga. Wale wachache wanaofanya hivyo wanaonekana wapinzani.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s